Tiba ya Malaria bado inatupiga chenga
Zipo taarifa kwamba Serikali iko mbioni kubadilisha sera na miongozo yake kuhusu tiba na uchunguzi wa ugonjwa wa malaria ili dawa mpya ya Artesunate ianze kutumika kutibu malaria kali badala ya Quinine. Kwa vyovyote vile, taarifa hizo zitaleta mkanganyiko na hofu miongoni mwa wananchi, kwani hatua hiyo ya Serikali inaweza kutafsiriwa kwamba dawa ya Quinine imeshindwa kutibu ugonjwa huo sugu na kwamba imekuwa ikitumiwa tu kama majaribio.
Wasiwasi na hofu inayoweza kuwagubika wananchi
kutokana na hatua hiyo ya Serikali inaeleweka. Kwanza, ugonjwa huo ndiyo
unaoua watu wengi zaidi katika nchi maskini kama Tanzania kuliko
ugonjwa mwingine wowote.
Hapa nyumbani, takwimu zinaonyesha kwamba watu
wapatao 80,000 hufariki dunia kila mwaka na wengine milioni 12 huugua
ugonjwa huo katika kipindi hicho. Kwa mujibu wa takwimu, asilimia 40 ya
wagonjwa ambao huripoti katika vituo vya afya kila mwaka hufanya hivyo
kwa kusumbuliwa na malaria.
Jambo la pili ni kwamba kubadilishwa kwa dawa hiyo
ya Quinine na badala yake kutumia Artesunate kunaweza kutafsiriwa na
wananchi wengi wa kawaida kwamba Quinine ambayo imekuwa ikitumika kwa
miongo mingi imeshindwa kutibu ugonjwa huo. Hofu itakuja pale wananchi
watakapoanza kujiuliza kuhusu madhara wanayoweza kuwa wameyapata
kutokana na matumizi ya dawa hiyo.
Hapo ndipo zitakapoibuka hisia kwamba miili yao imekuwa ikitumika muda wote huo kufanya majaribio ya dawa hiyo ya Quinine.
Ni jinsi gani basi wananchi watapokea ujio wa dawa
hiyo ya Artesunate katika mazingira kama hayo ni swali linalosubiri
wakati. Huko nyuma wananchi walishuhudia Serikali ikiziondoa sokoni dawa
kadhaa za kutibu malaria moja baada ya nyingine, ikiwa ni pamoja na
Chloroquine, Fansida na Dawa Mseto (Alu), kwa maelezo kwamba vimelea vya
ugonjwa huo vimekuwa sugu kwa dawa hizo. Unahitajika utafiti wa kutosha
kabla dawa hazijapitishwa kwa ajili ya matumizi ya binadamu.
Hoja tunayotaka kujenga hapa ni kwamba Serikali
imefanya makosa makubwa kuelekeza nguvu na rasilimali nyingi katika
kutafuta tiba ya malaria badala ya kutafuta chanzo chake kwa kutokomeza
mazalio ya mbu. Tumekuwa tukijidanganya kwa kudhani kwamba tutatokomeza
ugonjwa huo kwa kusambaza vyandarua au kubadilisha dawa za kutibu
malaria. Inaonekana tunafanya hivyo makusudi au hatujui kwamba gharama
za kuzuia malaria ni ndogo mno kuliko gharama za kuitibu.
Katika miaka ya 80 Serikali ya Japan ilibuni na
kufadhili mradi wa kunyunyizia dawa katika mazalio ya mbu hapa nchini.
Hata hivyo, mradi huo ulihujumiwa kwa sababu uligusa masilahi ya wakubwa
waliokuwa wakineemeka na uingizaji nchini wa dawa za kutibu malaria.
Ndiyo maana ugonjwa wa malaria unaendelea kudunda na kusababisha maafa
tuliyoyataja hapo juu.
Tunaambiwa Shirika la Maendeleo ya Taifa (NDC),
limepanga kujenga kiwanda mkoani Pwani cha kutengeneza dawa za
kuangamiza mazalio ya mbu. Jambo la ajabu ni kwamba mpango huo unapigwa
vita kila kona kwa sababu unagusa masilahi ya kundi fulani. Badala yake,
tunaambiwa Serikali inahaha huku na kule kuhakikisha sera na miongozo
yake kuhusu tiba ya Malaria zinabadilishwa haraka ili dawa mpya ya
Artesunate ianze kutumiwa mwezi huu badala ya Quinine. Bila shaka
wanaofaidika na mradi huo watakuwa wakisema kimya kimya: ‘Udumu ugonjwa
wa malaria’.
0 comments:
Post a Comment